THBUB yampongeza Rais kwa kuwafutia watu 61 adhabu ya kifo
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Bahame Tom
Nyanduga kwa niaba ya Tume na Wafanyakazi wote wa THBUB anachukua fursa
hii kumpongeza kwa dhati Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kufuta adhabu ya kifo kwa
watu 61 waliokuwa magereza mbalimbali nchini, wakisubiri utekelezaji wa
adhabu ya kifo dhidi yao.
Tume
inampongeza sana Mhe. Rais kwa uamuzi wake huo kwani unaendana na
Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Na. 62/149 la tarehe 18 Desemba
2007 linalozitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuta au
kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala.
Tume inatambua kwamba, kama alivyosema Mhe. Rais, msamaha huu haufuti adhabu ya kifo katika sheria za nchini.
Hivyo,
kutokana na mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 130(1) (g), Tume inapenda kuchukua
nafasi hii kuishauri Serikali kuona uwezekano wa kufuta adhabu ya kifo
na kuweka adhabu mbadala, ili iendane na Azimio la Umoja wa Mataifa
lililotajwa hapo juu.
Pia,
Tume inaisihi Serikali, hususan Idara yake ya Ustawi wa Jamii
kuwasaidia, na Wananchi kwa ujumla kuwapokea, wale wote waliopewa
msamaha ili waweza kuendelea na maisha yao kama raia wema katika jamii.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Desemba 9, 2017
No comments: