Benki ya Dunia yajipanga kukuza uchumi wa Tanzania na kupunguza umasikini
Mwakilishi
wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia
Bi. Bella Bird amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa benki hiyo imejipanga kuendelea kutoa
mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ili kukuza
uchumi na kupunguza umasikini.
Bi.
Bella Bird ametoa kauli hiyo leo tarehe 04 Desemba, 2017 Ikulu Jijini
Dar es Salaam na kubainisha maeneo ya kipaumbele kuwa ni miundombinu
hususani barabara na reli, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa nishati
ya umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na elimu kwa
kujielekeza katika ubora na kuhakikisha idadi ya wanaopata elimu
inaongezeka.
Maeneo
mengine ni kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa maji,
usimamizi bora wa ardhi, mawasiliano, huduma za fedha jumuishi, vituo
vya pamoja vya Serikali na kusaidia familia masikini.
Bi.
Bella Bird amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa usimamizi mzuri wa miradi
ya maendeleo inayotekelezwa na Benki ya Dunia na amemuahidi kuwa benki
hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika utekelezaji
wa miradi mingine.
“Mwaka
uliopita Benki ya Dunia imetoa mikopo nafuu yenye thamani ya Dola za
Marekani Bilioni 1.2 (Shilingi Trilioni 2.7) kwa Tanzania, fedha hizi
zimekwenda katika miradi mbalimbali na tunafurahi kuwa miradi hiyo
inakwenda vizuri na wananchi wanafurahia, kwa sasa tunapanga namna
tutakavyotoa mikopo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo katika
kipindi kijacho” amesema Bi. Bella Bird.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa
ushirikiano wake na Tanzania katika maendeleo na amemhakikishia Bi.
Bella Bird kuwa Serikali itazisimamia vizuri fedha zote zinazotolewa na
benki hiyo ili zilete matokeo yanayotarajiwa.
Mhe.
Rais Magufuli ameongeza kuwa maeneo yote ambayo benki hiyo imeyataja
kuwa kipaumbele katika fedha zitakazotolewa kuanzia sasa ni muhimu kwa
ustawi wa Tanzania na amesisitiza kuwa fedha zitakazotolewa kwa mkopo
zielekezwe katika maendeleo na sio vinginevyo.
“Naishukuru
sana Benki ya Dunia kwa kutuunga mkono, nitafurahi kuona mnaendelea
kutupatia fedha ambazo zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na kuleta
manufaa mapana na endelevu, badala ya kugawa fedha kwa watu na baadaye
nchi inakuja kuzilipa kwa kukusanya kodi za wananchi” amesisitiza Mhe.
Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli leo ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Desemba, 2017
No comments: