Header Ads

Waziri awataka wanafunzi kuitumia Vizuri Mikopo Wanayopewa

Naibu Waziri wa Fedha  Dk  Ashatu Kijaji amewataka wanafunzi wanaochukua mikopo ya elimu ya juu kwa ajili ya kujiendeleza kuitumia ipasavyo  kwa kusoma zaidi  ili watimize ndoto zao za elimu na hatimaye waliwezeshe taifa kupata wataalamu wa kutosha.

Amesema hayo  jana Desemba 3  kwenye  mahafali ya 19 ya Chuo cha Uhasibu Arusha  kikishirikiana na chuo kikuu cha Coventry cha Uingereza.

Alisema kuwa ,serikali kwa sasa inapambana katika kuhakikisha kuwa vijana wanapata mikopo ya kujiendeleza elimu ya juu hivyo ni vyema wanafunzi wote walionufaika na fursa ya kupata mikopo hiyo kuitumia kwa kusoma kwa makini ili kuliwezesha taifa kupata wataalamu wa nyanja mbalimbali.

"Nawaombeni Sana  mtumie fursa hiyo ya mikopo kujiendeleza zaidi katika fani mbalimbali ili tupate wataalamu watakaowezesha kuziba mianya mbalimbali ya wataalamu wanaohitajika ambao wamejiendeleza zaidi na waliobobea katika gani mbalimbali  "alisema Kijaji.

Kwa  upande wa Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo cha uhasibu Arusha, Rukia Adamu alisema kuwa, chuo hicho kimejikita katika kutoa mafunzo katika ngazi za Astashahada, shahada, stashahada na stashahada za uzamili  katika fani mbalimbali.

Alisema kuwa, chuo hicho pia kimeanza programu  maalum ya kujitolea kufundisha katika shule za sekondari zilizo Karibu na chuo kama mchango wao kwa taifa katika kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya hisabati, biashara  na teknolojia ya habari.

Rukia alisema kuwa, mojawapo ya mikakati ya chuo hicho ni kuanzisha kozi mbalimbali ambazo zinaendana na mahitaji ya soko kwa sasa ,huku chuo kikiendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kujua mahitaji ya watanzania ili kuweza kuanzisha kozi mbalimbali zinazokidhi mahitaji yao ili kuondoa adha wanayoipata watanzania kwenda kutafuta hizo kozi nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Naye Kaimu Mkuu wa chuo hicho cha uhasibu Arusha, Dokta Faraji Kasidi alisema elimu waliyopatiwa wahitimu hao utawawezesha kujiajiri wenyewe badala ya kuajiriwa katika nyanja mbalimbali walizosomea, huku ukizingatia uwezo wa serikali kuajiri wahitimu katika nyanja mbalimbali unapungua siku hadi siku.

Dk Kasidi amewataka wahitimu hao kutumia elimu yao kujitengenezea ajira, badala ya kuchagua kazi halali ambayo inawapatia kipato halali, hivyo akiwataka wote kuhakikisha wanaungana pamoja katika kuelekea nchi ya viwanda.

No comments:

Powered by Blogger.